Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Serikali ya Iraq, baada ya kuchapishwa kwa orodha katika Gazeti Rasmi la Wizara ya Sheria kuhusu kufungiwa mali za magaidi, zikiwemo za Hezbollah ya Lebanon na Harakati ya Wahuthi ya Yemen, imelazimika kujitokeza tena na kutangaza kuwa orodha hiyo inahitajika kufanyiwa marekebisho.
Kwa mujibu wa Shirika Rasmi la Habari la Iraq (INA), Kamati ya Kufungia Mali za Magaidi nchini humo imetangaza kwamba majina ya baadhi ya taasisi na watu yataondolewa kwenye orodha hiyo, ingawa haikubainisha kwa uwazi ni makundi gani yataondolewa.
Maendeleo haya yametokea baada ya gazeti la Al-Waqa’i linalomilikiwa na Wizara ya Sheria ya Iraq kuchapisha picha zinazoonesha kuwa serikali ya Iraq imeyaweka rasmi makundi ya Wahuthi na Hezbollah kwenye orodha ya mashirika ya kigaidi, na kutoa amri ya kufungia mali zao.
Hatua hii ya serikali ya Iraq imekuja katika mazingira ya shinikizo kubwa linaloongezeka kutoka Marekani, na pia kutokana na mahusiaono tata ya kisiasa kati ya Baghdad, Washington na Tehran. Iraq, ambayo ni mshirika wa kiuchumi wa Marekani, na wakati huohuo ni jirani na mshirika muhimu wa Iran (ambayo ina ushawishi mkubwa kupitia makundi ya wanamgambo wa Kishia na vyama vya siasa vyenye nguvu Baghdad), inajitahidi kuepuka kunaswa katikati ya mvutano wa kikanda.
Msimamo huu wa mkanganyiko unaashiria mizani nyeti na ngumu ambayo serikali ya Iraq inalazimika kuizingatia kati ya:
1-Kulinda uhusiano wake wa lazima na Iran, ambao uthabiti wake wa kiuchumi kwa kiasi kikubwa unategemea msaada wa Tehran,
2-Na wakati huohuo kudhibiti shinikizo la serikali ya Marekani la kutekeleza sera ya “shinikizo la juu kabisa” dhidi ya Iran.
Ripoti hizi zinachapishwa katika kipindi ambacho Iran iko chini ya mashinikizo makubwa zaidi ya kijeshi na kiusalama, kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel dhidi ya washirika wake kama Hezbollah na Hamas.
Your Comment